SHINYANGA: NAIBU WAZIRI WA MADINI MHE. DOTO BITEKO (MB) ATEMBELEA MGODI WA BUZWAGI
Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko (MB) amefanya ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji Madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazoukabili mgodi huo, Katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Ndg. Anderson Msumba, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Ndg. Timothy Ndaya, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Mhandisi Abdulrahman Milandu, Afisa Mgodi Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Modest Tarimo, Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini Mhandisi Frederick Mwanjisi, wataalam kutoka Wizara ya Madini.
Mara baada ya kufanya ziara na kupokea taarifa ya hatua za kufunga mgodi wa Buzwagi, Naibu Waziri Biteko alitoa maagizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na:- Mgodi kuwasilisha upya mpango wa ufungaji wa shughuli zake kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ili aweze kuwasilisha kwenye Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji wa Migodi kwa ajili ya kuidhinishwa ili utekelezaji wake uanze mara moja, pawepo na utaratibu wa kupitia upya kiwango cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa mazingira (rehabilitation bond) na kuweka mkakati wa kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi za wakazi wanaozunguka mgodi huo haziathiriki na ufungaji wa Mgodi husika.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliutaka uongozi wa mgodi huo kufuata sheria na kanuni za ufungaji wa mgodi kwa wakati na kuepuka kufanya kazi kwa zimamoto.
Meneja Mkuu wa Migodi ya Dhahabu ya Buzwagi na Bulyankulu, Benedict Buzunzu alisema kama mgodi wamepokea maelekezo na kuahidi kuwa watayafanyia kazi maelekezo waloyapata kutoka wizara ya Madini.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu kulia mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (MB) (kushoto) akimsikiliza Afisa Mgodi Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Modest Tarimo ( wa pili kulia) mara alipowasili kwenye ofisi yake iliyopo katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga. Kulia ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Mhandisi Abdulrahman Milandu.
Uchimbaji wa wazi wa dhahabu (open pit) ukiendelea katika Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Mtaalam kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi, Jonathan Joseph akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (Mb)
Sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Meneja Mkuu wa Migodi ya Dhahabu ya Buzwagi na Bulyankulu, Benedict Buzunzu (kushoto) akielezea mikakati ya Mgodi wa Buzwagi kwenye ufungaji wa shughuli zake kwa Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (Mb) (kulia)
Aidha Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko (MB) amewawahimiza wananchi kuwa na Imani na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi CCM, inayo ongozwa na Rais Mnyenyekevu Dkt John Pombe Magufuli na kuwataka kuamini kuwa rasilimali za Nchi zinalindwa kikamilifu na Serikali hasa upande wa Madini.
MWISHO.
@bazilmjungu#
Comments
Post a Comment