SERIKALI YATENGA SH. BILIONI 170 UJENZI MKONGO WA TAIFA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetenga shilingi bilioni 170 kwa ajili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa katika mwaka wa fedha 2021/2022.
“Lengo letu ni kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano kutumia miundombinu hii kuboresha huduma za mawasiliano nchini na kurahisisha ufikishwaji wa intaneti kwenye ofisi mbalimbali za sekta ya umma na binafsi”
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Oktoba 22, 2021) wakati alipofungua Mkutano wa Tano wa Mwaka wa TEHAMA Tanzania uliofanyika katika katika ukumbi wa mikutano wa AICC, jijini Arusha. Amesema fedha hizo zitawezesha kujenga kilomita 4,244 za Mkongo ili kufikisha jumla ya kilomita 12,563.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Habari, Sayansi na Teknolojia ya Habari isimamie kwa karibu mradi wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili wananchi wengi zaidi washiriki katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali.
“Hivi sasa Serikali imejenga kilomita 8,319 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi mwezi Septemba 2021. Malengo yetu kama Serikali ni kujenga hadi kilomita 15,000 ifikapo mwaka 2024/2025. Hili linahitaji uwekezaji mkubwa na Serikali imejipanga kuwekeza vilivyo lakini pia tunakaribisha wabia na wawekezaji katika eneo hili pamoja na maeneo mengine ya TEHAMA.”
Amesema kuwa miundombinu ya TEHAMA ni uti wa mgongo wa maendeleo ya kidijitali, hivyo nchi inahitaji kuongeza idadi ya watumiaji wa intaneti kufikia zaidi ya asilimia 80 nchi nzima kutoka asilimia 45. “Serikali imejiwekea lengo la kuongeza mtandao wa urefu wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kufikisha huduma bora na zenye gharama nafuu kwa wananchi wote.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali imedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye ramani ya Ulimwengu kama moja ya nchi ambayo TEHAMA imeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Comments
Post a Comment