TANZANIA IKO MIKONONI MWA MUNGU: WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA

Na: Bazil Mjungu - Lindi.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Tanzania iko mikononi mwa Mungu na ndiyo maana imeendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu na kimbilio la mataifa yaliyopoteza tumaini.


“Nchi hii imeshikwa na Mwenyezi Mungu na ni kwa sababu viongozi wa dini wanaendelea kuliombea Taifa hili, kwa hiyo na sisi tunalo jukumu la kuhakikisha kwamba nchi hii inabaki kwa salama,” Waziri Mkuu.


Mhe. Majaliwa Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Desemba 31, 2021) wakati akizungumza na waumini baada ya kushiriki ibada ya Ijumaa na kuzindua msikiti wa Nkowe, ulioko kata ya Nkowe, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Amesema Serikali zote tangu awamu ya kwanza hadi ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, zimeendeela kuheshimu uwepo wa dini nchini kwani miongozo na mafundisho yanayotolewa na viongozi wa dini mbalimbali yanawafanya waumini wao kuwa raia wema.


Mheshimiwa Rais alipoingia madarakani alikutana na Mababa Askofu wote wa nchi hii, lakini pia alikutana na masheikh wote kupitia BAKWATA ili kupata miongozo na baraka za kuongoza nchi hii.”


Aidha, Waziri Mkuu amewataka Watanzania wampe nafasi Rais Samia ya kufanya kazi kwa sababu amekuwa Serikalini kwa muda mrefu na anajua ni nini Watanzania wanatamani Serikali yao iwafanyie.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema madaraka yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu na yeye ndiye hupanga nani awe nani na kwa wakati gani. “Tuache tabia ya kuwafanya viongozi washindwe kufanya kazi zao kwa kuwatengenezea migogoro ya kila siku, tena mengine ya kusingizia tu.”

“Kila nafasi imetengenezwa na Mwenyezi Mungu na kila anayekwenda kuongoza Mwenyezi ndiye amesema wewe utakuwa pale. Na kama hajasema, hutokuwa; utatumia hela nyingi na zitapotea bure. Utakwenda na mambo mengine ya giza, lakini hutomudu. Mwenyezi Mungu keshasema huyu ni huyu, tuwaheshimu walioko kwenye nafasi za kuwatumikia Watanzania wafanye kazi zao kwa weledi.”

#wazirimkuu
#kassimmajaliwa
#bazotvonline
#bazotvnews

Comments

Popular posts from this blog

WASIFU BINAFSI JINA KAMILI: REHEMA SOMBI OMARY

IJUE FAIDA YA MSTARI WA IKWETA KUWA KARIBU NA NCHI YAKO

DC MTATURU Azindua Jengo la kituo cha huduma ya Mama na Mtoto Matare Ikungi Singida