BILIONI SITA ZIMETENGWA KWA AJILI YA MAADALIZI YA BARABARA KUTOKA SINGIDA HADI TANGA
SERIKALI imeahidi kuijenga kwa awamu barabara ya Handeni – Kiberashi –Kwamtoro hadi Singida yenye Kilomita 641 kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
Ahadi hiyo imetolewa Mei 5 bungeni na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Leonard Chamuriho wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu.
Katika swali lake mbunge huyo ameihoji serikali ni lini itajenga barabara hiyo ambayo ina manufaa kwa mikoa minne.
“Barabara hii tuna maslahi nayo , inaunganisha mikoa minne,ina historia katika nchi yetu na imefika sasa wakati serikali iamue kuijenga iishe kuliko kuanza kuwa na vipande vidogo vidogo,Je ni lini serikali itaanza kujenga barabara yote,?”.alihoji Mtaturu.
Akijibu swali hilo Mhandisi Chamuriho amesema kwa sasa wanaendelea kuijenga barabara hiyo kwa vipande kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Mwaka huu barabara hii imezingatiwa na tutajenga kipande kimoja na tutaendelea kuijenga kwa kulingana na upatikanaji wa fedha ,”.alisisitiza.
Awali akijibu swali la mbunge wa Chemba Mohammed Monni,Naibu waziri wa wizara hiyo Mwita Waitara amesema barabara hiyo ni muhimu na kukamilika kwake kutapunguza idadi ya magari yanayopita katika barabara kuu kuelekea Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa.
Amesema wizara hiyo kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo.
“Kwa sasa serikali ipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021 jumla ya Shilingi Bilioni sita zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami,na katika mapendekezo ya bajeti ya 2021/2022 barabara hii itazingatiwa,”alisema.
Mwisho.
Comments
Post a Comment